Higher Education Students' Loans Board
Wanafunzi wa shahada mwaka wa kwanza 30,311
Wanufaika 2,157 mikopo ya ‘Diploma’
Wanafunzi 588 kunufaika na ‘Samia Scholarship’
TZS 99.7 bilioni kutumika kuwagharimia mikopo, ruzuku TZS 2.9 bilioni
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo Jumatano (Oktoba 09, 2024) imetangaza awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi wenye sifa waliopangiwa mikopo na ruzuku kwa ajili ya mwaka wa masomo 2024/2025.
Makundi ya walionufaika katika Awamu ya Pili
Orodha iliyotangazwa leo inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na vyuo vya kati waliopangiwa mikopo kwa ajili ya Shahada ya awali (30,311) yenye thamani ya TZS 93.7 bilioni. Orodha ya awamu ya pili inafanya idadi ya jumla ya wanafunzi 51,645 waliopangiwa mikopo katika awamu ya kwanza na awamu ya pili kwa ajili ya kugharimia masomo yao ya shahada ya awali ikiwa na thamani ya TZS 163.8 bilioni. Kati ya wanafunzi hao, wanafunzi wa kike ni 22,216 (sawa na 43%) na wa kiume 29,429 (sawa na 57%)
Awamu hii ya pii inajumuisha pia mikopo ya Stashahada (Diploma) kwa wanafunzi wapatao 2,157 yenye thamani ya TZS 5.6 bilioni. Wanafunzi wengine 45 ni wa shahada ya uzamili waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 205.6 milioni na wanufaika 16 wa Shahada ya Uzamivu waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 215.6 milioni.
Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Tatu
HESLB inaendelea kupokea taarifa za udahili kuwezesha kupanga mikopo na kutangaza Awamu ya tatu ya orodha ya wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2024/2025 itakayotangazwa siku chache zijazo ili kuwawezesha wanafunzi waliopangiwa mikopo kuendelea na taratibu za kujisajii katika vyuo walikodahiliwa.
Samia Scholarship
Taarifa hii pia ina idadi ya wanafunzi 588 wa shahada ya awali watakaonufaika na fursa za ‘Samia Scholarships’ kwa mwaka huu 2024/2025, ambao wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya TZS 2.9 bilioni. Wanafunzi hawa ni wenye ufaulu wa juu katika tahasusi za sayansi na waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali kwenye fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na hisabati na sayansi za Tiba.
Wito
HESLB inawakumbusha waombaji wa mikopo na ruzuku wenye sifa kwa mwaka 2024/2025 ambao bado hawajapangiwa mikopo au ruzuku, kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia ‘SIPA’ wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo na ruzuku zikiendelea.
Taarifa hii pia inapatikana www.heslb.go.tz na katika kurasa za mitandao ya kijamii ya Instagram, Facebook na X (zamani Twitter) kwa jina la HESLB Tanzania.
Imetolewa na:
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Jumatano, Oktoba 09, 2024