Higher Education Students' Loans Board
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema yupo tayari kushiriki katika maandalizi na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kutambua kuwa Bodi hiyo imewekeza kwenye maendeleo ya watu.
Mhe. Chalamila ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia aliyefika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa leo (Januari 22, 2025) kujitambulisha rasmi na kutambulisha Maadhimisho ya Miaka 20 ya HESLB ambayo yanajumuisha maonesho, vituo vya huduma, mbio za hisani na mkutano wa kilele utakaofanyika Februari 17, 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es salaam.
“Miaka hii ishirini siyo jambo dogo … ni jambo la kujivunia kwamba mmewekeza kwenye maendeleo ya watu … ni kitu ambacho kinatakiwa ili kuendeleza maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa kama Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere”, amesema Mhe. Chalamila.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam ameeleza kuwa ni muhimu kutumia maadhimisho hayo kuonesha athari chanya za kuanzishwa kwa HESLB hususan kwa wanufaika, wazazi na wadau wengine wakiwemo wamiliki wa vyuo ambao wamenufaika na uwepo wa Bodi ya Mikopo kuwezesha kufikia ndoto zao.
Licha ya Mkutano wa kilele, RC Chalamila ameonesha kuvutiwa na mbio za hisani zitakazofanyika Februari 15, 2025 jijini Dar es salaam na kuongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambapo amesema ataungana na HESLB kufikisha ujumbe wa hamasa kwa wananchi kupitia mkutano na wanahabari siku chache zijazo.
“Kuwe na Press Conference kueleza ni kwa nini mmeamua kuwa na maadhimisho haya na jinsi gani mtu anaweza kushiriki … uwepo pia mkakati wa kuchangisha kwa waliokwishanufaika, kupitia simu au njia nyingine rahisi”, amesisitiza Mhe. Chalamila.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia aliyeteuliwa kushika wadhifa huo na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Februari mwaka uliopita, alieleza lengo la kufika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kuwa ni kujitambulisha rasmi na kutambulisha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayofanyika na kuwaleta pamoja wadau wa elimu ya juu.
Maadhimisho ya miongo miwili tangu kuanzishwa kwa HESLB yanaongozwa na Kauli mbiu isemayo “Athari Chanya, Ubunifu na Huduma”, ikiakisi mageuzi makubwa yaliyofanyika katika kugharimia wanafunzi zaidi ya 830,000 wa elimu ya juu nchini kwa thamani ya TZS 8.2 Trilioni.