Higher Education Students' Loans Board
WANAFUNZI 4,676 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 15.5 BILIONI KWA RUFAA
Upangaji wa mikopo kwa mwaka 2024/2025 wafikia mwisho
Wanafunzi 4,676 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 15.5 bilioni baada ya rufaa zao kufanikiwa katika mwaka wa masomo 2024/2025.
Taarifa iliyotolewa leo (Jumanne, Disemba 03, 2024) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia imesema kuwa wanafunzi 4,183 ni wa mwaka wa kwanza ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 13.8 bilioni na wanafunzi wengine 493 ni wa mwaka wa pili na kuendelea ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 1.7 bilioni kwa njia ya rufaa.
Aidha, taarifa hiyo ya Dkt. Kiwia inajumuisha wanafunzi 3,934 wa mwaka wa pili na kuendelea ambao wamepangiwa mikopo kwa mara ya kwanza yenye thamani ya TZS 12.4 bilioni.
“Jumla ya wanafunzi 86,646 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 273.46 bilioni; kati yao wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 79,573 na wanafunzi wa mwaka wa pili na kuendelea waliopangiwa mikopo kwa mara ya kwanza ni 7,073”, imeeleza taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Kiwia imehitimisha kwa kueleza kuwa upangaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025 umefika kikomo na kwamba waombaji ambao hawakufanikiwa kupata wanashauriwa kuomba mikopo dirisha wakati litakapofunguliwa mwaka 2025/2026.
Taarifa hii pia inapatikana kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii (Facebook, Instagram na X) kwa jina la HESLB Tanzania.