Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


16
December 2024

PROF. MKENDA AZINDUA 'HESLB APP'

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, leo (Jumatatu, Disemba 16, 2024) amezindua mfumo wa huduma kidigitali unaofahamika kwa jina la ‘HESLB APP’ ili kurahisisha huduma za utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi inayotolewa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Hafla fupi ya Uzinduzi wa ‘HESLB App’ imefanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, maafisa mikopo wa vyuo vikuu na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa ‘HESLB App’, Prof Mkenda amesisitiza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuona kuwa mamlaka zote za serikali katika ngazi mbalimbali zinaongeza ubunifu na ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

“Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha inaweka mazingira ya kutoa huduma bora na kwa urahisi kwa wananchi na hasa kwa kutumia mifumo ya kidigitali…”, amesisitiza Prof. Mkenda.

Aidha, kuhusu upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kati, Prof Mkenda amewasisitiza waombaji mikopo kuweka taarifa sahihi na kamilifu kwenye maombi yao ya mikopo kuthibitisha uhitaji wao ili waweze kunufaika na mikopo ya elimu kupitia HESLB.

Awali, akimkaribisha Prof. Mkenda, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB Prof. Hamisi Dihenga amesisitiza umuhimu wa ‘HESLB App’ na kuongeza kuwa elimu zaidi itolewe kwa wanafunzi na wanufaika wa mikopo ili waweze kuitumia vizuri ‘App’ hiyo na kurahisisha upatikanaji wa huduma. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia ametoa wito kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo vyuoni na wanufaika wa mikopo waliohitimu vyuo, kujisajili na kuanza kupata huduma kwa urahisi kupitia ‘HESLB App’.

“Kupitia HESLB App, wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu na kati wanapata fursa ya kujisajili kwenye mfumo wa ‘Digital Disbursement’ maarufu DiDiS, unaowawezesha kupokea malipo yao kwa njia ya kidigitali kwa usahihi, urahisi, na haraka…” amefafanua Dkt. Kiwia.

‘HESLB App’ ni mfumo wa kidijitali unaotumia simu janja (Android na iOS) ambao umetengenezwa na wataalam wa ndani wa kitengo cha TEHAMA cha HESLB, kwa ajili ya kurahisisha huduma za utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi hapa nchini ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na HESLB ili kurahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wateja wake.