Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


17
February 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA AHITIMISHA MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA HESLB

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) leo Februari 17, 2025, amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Mhe. Majaliwa amesisitiza kuhusu HESLB kuboresha mahusiano zaidi na taasisi za kifedha ili kuongeza ufanisi na kutoa elimu ya kutosha kwenye shule za sekondari zenye kidato cha tano na sita kuhusu sifa, vigezo na taratibu za utoaji wa mikopo hii kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na vya kati nchini. 

“Naishauri Bodi ya Mikopo ikae pamoja na taasisi za kifedha ili kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na kuwezesha watanzania wengi kusoma elimu ya juu…lakini vilevile elimu kuhusu mikopo itolewe kwa wanafunzi wa sekondari ambao hao ndio haswa walengwa wa mikopo hii ya elimu ya juu’’, amesema Mhe. Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ambaye pia ni mnufaika wa mikopo ya elimu ya juu, amewashukuru na kuwapongeza sana viongozi watangulizi walioona mbali na kuamua kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo.

“Ninawapongeza viongozi wetu wa nchi, kwa kuendelea kuweka kipaumbele cha kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu katika awamu zote tangu Bodi hii ilipoanzishwa. Dhamira njema ya Viongozi wetu imewezesha hadi sasa wanafunzi 830,000 kunufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 8.2 tangu kuanzishwa kwa Bodi’’, amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (MB) amesema kuwa wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani alikuta fedha zinazotolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 464 na na sasa imefikia shilingi bilioni 787.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani bajeti ya mikopo ilikuwa shilingi bilioni 464, aliagiza fedha kwa ajili ya mikopo ziongezwe, na tuliongeza hadi kufikia bilioni 570, tukaendelea hadi shilingi bilioni 654 na sasa ni shilingi bilioni 787”, ameeleza Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha miaka 20, viongozi katika awamu zote wamefanya kazi kubwa katika kuhakikisha Bodi ya Mikopo inajiongezea uwezo ili kuwahudumia vijana wengi zaidi wa Kitanzania.

“Niliyoyaona na kuyasikia yamenifurahisha sana, uongozi ni kazi ya kupokezana kijiti, mwenzako anakimbia mpaka hapa, wewe unapokea unakimbia mpaka pale … nilikabidhiwa na Mzee Mkapa nikafanya nilichoweza, tukaachia awamu ya tano ikafanya ilichokiweza na ikaiachia awamu ya sita … na sasa mambo mazuri Zaidi, kazi iendelee”, amesema Dkt. Kikwete.

Maadhimisho hayo ya Miaka 20 ya HESLB iliyoanzishwa kwa Sheria mwaka 2004, yalianza tangu tarehe 10 Februari 2025 kwa kutoa huduma kwenye kliniki katika mikoa 7 nchini, lengo likiwa ni kutoa elimu na huduma kwa wadau mbalimbali kuhusu masuala ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Baada ya kliniki hizo, lilifuatia tukio la mbio za hisani tarehe 15 Februari, 2025 zilizoanzia na kuishia katika viwanja vya Farasi jijini Dar es Salaam.

Kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya HESLB kinafanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 17 hadi 18 Februari, 2025, kwa kukutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi ili kutathmini na kujadili mambo ya kimkakati kuhusu safari ya HESLB ya miaka 20 na maboresho yanayopendekzwa kufanyika ili kuongeza ufanisi zaidi kwa miaka ijayo.