Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


8
March 2025

Rais Samia anogesha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake

- Azungumzia kuongezeka kwa bajeti mikopo ya wanafunzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (leo Jumamosi, Machi 8, 2025) amehitimisha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa ngazi ya kitaifa na kuelezea jinsi serikali ilivyowekeza kwenye elimu kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu ambapo amegusia kuhusu ongezeko la bajeti ya mikopo toka mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025.

“Bajeti ya mikopo imeongezeka toka shilingi bilioni 450 kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 787 kwa mwaka huu wa 2024/2025. Kwa sasa pia serikali inatoa mikopo kwa ngazi ya stashahada … na katika kuongeza hamasa kwenye masomo ya sayansi, tumeanzisha Samia Scholarship kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwenye mitihani ya kidato cha Sita. Vilevile, tumejenga Shule maalumu za Sayansi kwa ajili ya watoto wa kike … na hadi sasa kuna shule angalau moja kwa kila mkoa”, ameelezea Mhe. Rais.

Katika hatua nyingine Rais Samia amesisitiza kuwa na serikali inayozingatia usawa wa kijinsia katika sekta zote na akaongeza kuwa, “…Nitaendelea kusisitiza kuwepo na usawa wa kijinsia katika sekta zote nchini,” amesisitiza Rais.

 Akifunga hotuba yake Mhe. Rais Samia ametoa rai kwa wanawake na wanaume kuendelea kushirikiana na kulinda amani na utulivu wa taifa la Tanzania.

Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa yamefanyika leo Machi 8, 2025, katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo “Wanawake na wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”, yamepambwa na shamrashamra mbalimbali yakiwemo maonesho ya taasisi za serikali na binafsi yaliyofanyika kwa wiki nzima katika mkoa wa Arushakwa lengo la kutoa huduma na kuelimisha umma.

Watumishi Wanawake kadhaa wa HESLB kutoka katika kanda saba ambapo ofisi za HESLB zipo, wameshiriki katika maadhimisho hayo jijini Arusha.