Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


30
July 2025

Wazazi Bukoba Wajitokeza kwa Wingi Kupata Elimu ya Uombaji Mikopo

Wazazi na walezi wa mji wa Bukoba wamejitokeza kwa wingi leo (Jumatano, Julai 30, 2025) kupata elimu ya uombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/2026 inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na wadau wengine wa kimkakati.

Wazazi walioshiriki katika mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Bukoba, wamepongeza hatua hiyo ambayo pia imewajumuisha wadau wengine wanaoshiriki katika hatua za kukamilisha maombi ya mikopo wakiwemo Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Anwani ya Makazi (NaPA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Posta (TPC).

Pamoja na kupata fursa ya kuuliza na kujibiwa maswali yao ana kwa ana, baadhi ya wazazi wamependekeza kuwa mara nyingine elimu hiyo ifikishwe kwa wadau walioko maeneo ya nje ya mji wa Bukoba ikiwemo Wilaya ya Karagwe iliyopo umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka Bukoba mjini.

Awali akifungua mafunzo hayo yaliyowalenga pia wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na stashahada, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Yohana Sima, amewataka vijana waliohitimu kidato cha sita na wanaoendelea na masomo kwa sasa, kutumia vizuri fursa ya kugharimiwa na serikali katika ngazi ya vyuo vya kati na elimu ya juu kwa kusoma kwa bidii na kukumbuka kurejesha mikopo hiyo baada ya kuhitimu ili kuwasomesha wanafunzi wengine wahitaji.

“Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeizingatia sekta ya elimu kwa kuendelea kuongeza bajeti mwaka hadi mwaka … mwaka wa masomo ulioisha 2024/2025, bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ilikuwa TZS bilioni 787, mwaka huu wa 2025/2026, bajeti hiyo imeongezeka na kufikia TZS bilioni 916. Ndani ya kipindi hicho pia kiwango cha fedha za kujikimu kwa siku kimepanda kutoka Shilingi 8,500 hadi shilingi 10,000. Hayo mambo ni makubwa na ya kihistoria kwa nchi yetu”, ameeleza Mhe. Sima.

Naye Mwalimu Raymund Mutakyahwa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukoba yenye kidato cha I hadi VI, ameshukuru kwa shule hiyo anayoiongoza kuwa kituo cha kutolea elimu ya uombaji mikopo akisema kuwa kwake ni mtaji na fursa kwa wanafunzi wake kuelimishwa pia wakati wakikaribia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Ratiba ya leo ya utoaji wa elimu ya taratibu za uombaji mikopo imefanyika pia Iringa mjini katika Shule ya Sekondari Lugalo, Babati Mkoani Manyara na Mtwara katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara.

Katika maeneo yote, maafisa wa HESLB, benki ya CRDB, NaPA, NIDA na RITA wameshirikiana kuwaelimisha wazazi, walezi, watoa huduma za internet na wanafunzi wanaoomba mikopo ili kuepuka makosa yanayoweza kujitokeza na kumkosesha mkopo mwanafunzi mwenye sifa kwa kutoomba mkopo kwa usahihi.

Ratiba ya utoaji elimu kesho (Alhamisi, Julai 31, 2025) itaendelea kwenye vituo mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Morogoro na Tanga.