Higher Education Students' Loans Board
Lajadili maboresho ya utendaji na utatuzi wa changamoto za wafanyakazi
Baraza la Wafanyakazi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) limekutana leo mjini Morogoro kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo, huku Menejimenti ikitoa majibu ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe wa baraza hilo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo, amesema Baraza ni chombo muhimu kinachosaidia kuongeza uwajibikaji na ushirikiano kati ya Menejimenti na watumishi.
“Kupitia Baraza la Wafanyakazi tunapata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa watumishi wetu. Hii inatupa fursa ya kutatua changamoto zao na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi,” amesema Dkt Kiwia.
Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa baraza, Bi. Dorah Konga, amesema baraza limekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha sauti za watumishi zinasikika.
“Hii ni nafasi ya kipekee kwa sisi wafanyakazi kueleza changamoto zetu na kutoa mapendekezo. Tunashukuru kwa majibu na hatua zinazochukuliwa na Menejimenti,” amesema Bi. Dorah.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Habari, Ufundi Stadi na Utafiti (RAAWU), Tawi la HESLB, Bw. Daud Elisha amebainisha kuwa majadiliano ya kina kwenye Baraza la Wafanyakazi ni muhimu sana kwa kuwa yanagusa maslahi ya watumishi na kuboresha mazingira yao ya kazi.
“Maslahi na mazingira bora ya kazi ni kichocheo cha kuongeza ufanisi katika kazi za taasisi. Tumetoa maoni kadhaa ambayo Menejimenti imeahidi kuyafanyia kazi,” amesema Bw. Elisha.
Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kiutendaji linalowawezesha watumishi kushiriki katika maamuzi ya kikazi. Kwa mujibu wa Menejimenti ya HESLB, chombo hicho kimeendelea kuwa nguzo ya mshikamano, uelewano na ari ya kufanya kazi kwa pamoja katika kutimiza majukumu ya kitaasisi.