Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


17
September 2025

HESLB YAWASILISHA FEDHA ZA VIFAA VYA MAABARA SHULE YA SEKONDARI HASNUU MAKAME

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), Dkt. Mwanakhamis Adam Ameir, ameongoza hafla ya makabidhiano ya TZS 10,000,000/= zilizotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika Shule ya Sekondari Hasnuu Makame, Mkoa wa Kusini Unguja.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyopambwa pia na burudani ya shairi mahususi la tukio hilo, Dkt. Mwanakhamis ameishukuru HESLB kwa msaada huo na kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha hizo kwa manufaa ya wanafunzi na walimu.

“Naishukuru HESLB kwa msaada huu ambao utaenda kusaidia kupata vifaa vya maabara katika skuli hii ya Hasnuu Makame. Nasisitiza fedha hizi zitumike kwa uadilifu na umakini mkubwa ili kuhakikisha vifaa muhimu vinapatikana na wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo. Huu ni uwekezaji kwa wanafunzi … na taifa linawaangalia kama viongozi na wataalamu wa kesho,” amesema Dkt. Mwanakhamis.

Dkt. Mwanakhamis ameongeza kuwa Serikali inathamini ushirikiano wa taasisi kama HESLB na jamii katika kukuza elimu. “Tunatoa pongezi na shukrani za dhati kwa msaada huu wenye tija. Tunaomba HESLB iendelee kushirikiana na jamii katika kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuboresha elimu inatekelezwa ipasavyo,” amesema Dkt. Mwanakhamis.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema msaada huo umetokana na michango ya wadau mbalimbali wa elimu waliyoitoa kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya HESLB, mwezi Februari mwaka huu.

“Kupitia michango ya wadau kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya HESLB, tumeweza kutenga sehemu ya fedha kusaidia shule hii kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara. Hii ni ishara ya dhamira yetu ya kushirikiana na jamii katika kuboresha elimu ya sekondari nchini,” amesema Dkt. Kiwia.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Hasnuu Makame, Mwl. Bakari Mohammed Ali, ameishukuru serikali kupitia HESLB kwa msaada huo ambao amesema utasaidia wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo katika masomo ya Sayansi.

Msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya HESLB iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, ambapo shule mbili za sekondari, moja kutoka Tanzania Bara na nyingine kutoka Zanzibar zimenufaika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na walimu, wanafunzi, viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na wadau wa elimu, ambapo imesisitizwa kuwa msaada huo utakuwa chachu ya kuboresha mazingira ya kujifunza kwa vitendo kwa wanafunzi wa Shule ya Hasnuu Makame.