Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo imekabidhi kiasi cha Shilingi Milioni kumi (TZS 10,000,000) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara katika Shule ya Sekondari Temeke, hatua ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua kiwango cha ufaulu katika masomo ya sayansi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ambapo kupitia michango ya wadau, HESLB imeweza kutenga sehemu ya fedha kwa ajili ya kusaidia shule mbili za sekondari, moja ya Tanzania Bara na nyingine ya Zanzibar, kwa kuwapatia msaada wa fedha kwa ajili ya vifaa vya maabara.
“Pamoja na kuwa tunatimiza ahadi tuliyoitoa, msaada huu pia ni sehemu ya jitihada za HESLB katika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya elimu, hususan masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). Tunatambua kuwa taifa letu haliwezi kufikia uchumi wa kati wa viwanda bila kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia kuanzia ngazi za chini,” amesema Dkt. Kiwia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Mwalimu Ingia Madika Mtenga, ametoa shukrani kwa Serikali, HESLB na wadau wote wa elimu kwa mchango huo, akieleza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya mabadiliko makubwa kwa wanafunzi kwa kuwawezesha kujifunza kwa vitendo kwa ufanisi mkubwa.
“Fedha hizi zitasaidia kufanya maboresho makubwa na kununua vifaa muhimu vya maabara, jambo litakalowasaidia wanafunzi wetu kujifunza kwa vitendo na kuongeza ufaulu katika masomo ya sayansi,” amesema Mwalimu Mtenga.
Akizungumzia vifaa vitakavyoongezwa katika maabara ya shule hiyo, Mwalimu Mtenga ameeleza kuwa wamepanga kununua vifaa vitakavyosaidia katika ufundishaji na kujifunza masomo ya Bailojia (Biology), Kemia (Chemistry) na Fizikia (Physics).
“Tunatambua jitihada za Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa kuwawezesha wanafunzi katika elimu ya kati na ya juu. Fedha hizi tulizopokea leo zitasaidia kuongeza vifaa kama mashine za kuchuja maji na ‘models’ zinazoonyesha mfumo wa binadamu kwa maabara ya Baiolojia. Tunashukuru na tunaipongeza Serikali kupitia Bodi ya Mikopo, na tunamtakia kila heri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake katika kuimarisha sekta ya elimu,” ameeleza Mwalimu Mtenga.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, amewasihi wanafunzi kusoma kwa juhudi na kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo serikali inatoa kwao hasa kwa upande wa sayansi ikiwemo “Samia Scholarship”, ambayo ni mahsusi kwa ajili ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita.
Makabidhiano hayo yameelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa HESLB wa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kuchangia katika maboresho ya mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Wengine walioshuhudia hafla hiyo walikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Mtendaji wa Kata ya Sandali ilipo shule hiyo ya Sekondari Temeke, menejimenti ya HESLB, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Temeke.