Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


30
June 2025

DKT. KIWIA AFUNGA MWAKA WA FEDHA 2024/2025 KWA KIKAO CHA WAFANYAKAZI NA KUTOA MWELEKEO WA MWAKA MPYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, leo Juni 30, 2025 ameongoza kikao maalum cha ndani cha kufunga mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA, Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha watumishi wote wa HESLB kutoka katika vitengo, idara mbalimbali na kanda, Dkt. Kiwia amewapongeza watumishi kwa juhudi na mchango wao katika kutekeleza majukumu ya taasisi kwa ufanisi. “Nawapongeza watumishi wote kwa kuchapa kazi kwa juhudi na kujitoa ili kuhakikisha taasisi yetu inatimiza malengo yake kwa mwaka huu unaoisha wa 2024/2025”, amesema Dkt. Kiwia

Dkt. Kiwia ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka wa fedha unaomalizika, hususan katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. “Jumla ya shilingi bilioni 787 zimetolewa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kuwanufaisha takribani wanafunzi wapya 81,000…’’, ameeleza Dkt Kiwia.

Kwa mwaka wa fedha ujao wa 2025/2026, unaoanza rasmi kesho, Julai 1, 2025, Dkt. Kiwia ameweka wazi kuwa serikali imeongeza bajeti ya mikopo hadi kufikia shilingi bilioni 916, ambazo zitatolewa kwa jumla ya wanafunzi 252,000, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaoendelea na masomo pamoja na wanufaika wapya.

Kuhusu makusanyo ya mikopo kutoka kwa wanufaika wa zamani, Dkt. Kiwia amesema kuwa HESLB imefanikiwa kuongeza makusanyo kutoka shilingi bilioni 177 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia bilioni 194 katika mwaka wa 2024/2025. Vilevile amewajulisha watumishi kuwa lengo jipya la makusanyo lilipangwa na serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026 ni shilingi bilioni 210.

”Nawasihi watumishi wote tuongeze juhudi zaidi katika kazi zetu ili kufikia lengo jipya la ukusanyaji wa mikopo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 ambalo litakuwa bilioni 210…”, amesisitiza Dkt. Kiwia

Akizungumzia masuala ya rasilimaliwatu, Dkt. Kiwia amesema HESLB ina jumla ya watumishi 291, wakiwemo wanaume 161 na wanawake 130. Amesisitiza kuwa mafunzo mbalimbali yamekuwa yakiendelea kutolewa kwa watumishi ili kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, Dkt. Kiwia ametaja kuwa HESLB imeendelea kuboresha mifumo mbalimbali ya TEHAMA, hususan ile ya utoaji huduma kwa wateja, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma na kusogeza huduma hizo karibu zaidi na walengwa. “Kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 tutaendelea kuhakikisha huduma zetu zote zinapatikana kwa njia ya mtandao na kuwa taasisi bora ya mfano katika utoaji wa huduma bora zaidi na zinazopatikana kwa urahisi”, amesisitiza Dkt. Kiwia

Katika kuongeza morali na motisha kwa watumishi, Dkt. Kiwia amesema taasisi imeboresha maslahi ya wafanyakazi ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi na kuwezesha kufikia malengo ya taasisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi - RAAWU tawi la HESLB, Bw. Daud Elisha, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa niaba ya watumishi wote kwa uongozi wake imara na utayari wa kusikiliza na kushughulikia maslahi ya wafanyakazi. Ameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na menejimenti ili kuhakikisha watumishi wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi na kuwahudumia wateja kwa ubora unaostahili.