Higher Education Students' Loans Board
Zanzibar, Jumamosi, Machi 29, 2025
HESLB imepongezwa kwa kusimamia mikopo ya wanafunzi na kuwezesha takriban watanzania milioni moja kupata elimu na ujuzi katika fani mbalimbali zinazowawezesha kujenga uchumi na maendeleo ya nchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, siku ya Jumamosi, Machi 29, 2025 alipokuwa Mgeni rasmi katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na HESLB hoteli Verde, Zanzibar.
“Idadi ya watanzania waliokwishasomeshwa siyo ndogo … tunahitaji wataalamu katika fani mbalimbali ili waweze kutekeleza mipango inayoandaliwa na serikali …”, amesema Mhandishi Zena.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, mashirika na taasisi binafsi, iliandamana na utoaji wa tuzo kwa viongozi kadhaa kutambua juhudi na michango yao tangu kuanzishwa kwa HESLB miaka 20 iliyopita. Viongozi waliotunukiwa ni pamoja na Rais wa awamu ya sita wa Zanzibar Dkt. Mohamed Ali Shein, Dkt. Mohamed Gharib Bilal aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohamed Mussa. Tuzo za viongozi hao zilipokelewa kwa niaba yao na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma.
Awali wakati akitoa neno la ukaribisho na shukrani, Mkurugezi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia aliwashukuru wote waliotikia mwaliko na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kutimiza malengo ya serikali ya kugharimia vijana wengi wa kitatanzania kupitia mikopo ya elimu.
Kila mwaka katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan, HESLB huandaa Iftar na kuwaalika viongozi wa serikali na wadau wa kimkakati ili kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuonesha ukarimu.