Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewakumbusha wanafunzi wanaoomba mkopo wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kusoma miongozo na kuizingatia ili kuepuka kuwasilisha maombi yenye makosa.
Katika mkutano wake na wanahabari leo (Alhamisi, Agosti 1, 2024), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema ingawa dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufungwa Agosti 31 mwaka huu, tathmini ya siku 60 zilizopita inaonesha maombi yanayowasilishwa hayazingatii miongozo iliyotolewa.
“Dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao kwa makundi mbalimbali lipo wazi kwa siku 90 kuanzia Juni 1 mwaka huu … na tumepokea zaidi ya maombi 40,000 lakini yaliyo kamili ni chini ya 25,000 … tunashauri waombaji wasome miongozo ambayo inapatikana katika tovuti yetu (www.heslb.go.tz),” amesema Dkt. Kiwia.
Makundi ya wanafunzi wanaoomba mkopo ni wanafunzi wa shahada za awali (Undergraduate Degrees); wanafunzi wa Stashahada (Diploma); wanafunzi wa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Uanasheria (Post Graduate Diploma in Legal Practice); na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu (Masters and PhD students).
Kuhusu ‘Samia Skolashipu’ kwa 2024/2025
Kuhusu fursa za Skolashipu za Samia ambazo zinawalenga wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika tahasusi za sayansi katika mitihani ya kidato cha sita, Dkt. Kiwia amesema orodha ya wanafunzi hao itaanza kupatikana katika tovuti ya HESLB kuanzia kesho, Ijumaa, Agosti 2 na wataweza kuanza kuomba Jumamosi, Agosti 3.
“Tumeshapokea orodha ya wanafunzi 700 wenye ufaulu wa juu kutoka kwa Wizara yetu na tunakamilisha utaratibu ili kuiweka orodha na utaratibu wa kuomba kwenye tovuti na kuruhusu mifumo ya uombaji ili waweze kuomba fursa za ‘Samia Scholarships’ kuanzia keshokutwa, Agosti 3,” amesema Dkt. Kiwia.
Orodha hii inajumuisha wanafunzi 17 wenye mahitaji maalum; wanafunzi wavulana 394 na wasichana 289 ambao wana ufaulu wa juu zaidi katika tahasusi za sayansi katika mitihani ya kidato cha sita inayoendeshwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA).
Kuhusu fursa za BURE za mafunzo ya kuongeza ujuzi
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amewakumbusha wanafunzi-wahitimu na waliopo mwaka wa mwisho wa shahada za TEHAMA na sayansi ya kompyuta (ICT and Computer-related degrees) kutumia siku nne zilizobaki kujisajili na kuomba fursa za mafunzo kupitia https://dlt.adanianlabs.io.
“Tuna makubaliano na taasisi ya Adanian Labs ambayo yanalenga kutoa mafunzo ya bure kwa njia ya mtandao kwa wanufaika wetu ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa na kuwa na kipato cha kurejesha mkopo wetu … watumie siku nne hizi kujisajili na kupata fursa za mafunzo,” amesema Dkt. Kiwia.
Kuhusu Bajeti ya Mikopo
Katika mwaka wa masomo 2024/2025, Serikali imetenga TZS 787 bilioni ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 245,000 wakiwemo wanafunzi 80,000 wa mwaka wa kwanza.
Katika mwaka wa masomo 2023/2024, Serikali imetoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 224,056, wakiwemo wanafunzi 78,979 wa mwaka wa kwanza.