Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


16
February 2024

HESLB, SAFAG ya Uswizi zaanza mazungumzo kuongeza vyanzo vya fedha

HESLB, SAFAG ya Uswisi zaanza mazungumzo kuongeza vyanzo vya fedha

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dr. Bill Kiwia amekutana na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Swiss Alternative Financing (SAFAG) yenye makao makuu yake jijini Geneva, Uswisi Bi. Leyla Baghirzade na kufanya mazungumzo yaliyolenga katika kuangalia maeneo ya ushirikiano katika ugharimiaji wa elimu ya juu nchini.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo (Ijumaa, Februari 16, 2024) katika Ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA jijini Dar es salaam. SAFAG ni taasisi inayojishughulisha na masuala ya kifedha ikilenga kuwakutanisha wawekezaji wenye fedha kutoka ulaya na taasisi au mashirika mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto zinazozikabili taasisi hizo.

Akizungumza katika kikao hicho, Dr. Kiwia amemwelezea Bi. Baghirzade jitihada ambazo Serikali imeendelea kuchukua ikiwemo kuongeza bajeti ya mikopo kila mwaka ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kupitia HESLB.

“Kwa sasa, Serikali kupitia HESLB inagharimia takribani asilimia 70 ya wanafunzi wote wa elimu ya juu na fedha zinatoka Wizara ya Fedha pekee, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mashirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo SAFAG,” amesema Dkt. Kiwia.

Naye Mtendaji Mkuu wa SAFAG, Bi. Baghirzade ameeleza kufurahishwa na jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuzalisha nguvu kazi na kuahidi kuwa taasisi itatoa ushirikiano ili kuhakikisha HESLB inaanzisha ushirikiano rasmi na taasisi za fedha zinazofanya kazi na SAFAG ili kupunguza utegemezi Serikalini.

Kikao hicho kimehudhriwa na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya HESLB wakiwemo Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na TEHAMA, Benedicto Cosmas; Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Neema Kuwite; Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo, Dkt. Peter Mmari; na Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Wakili Agatha Mchome.