Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


10
November 2021

HESLB YAONGEZA SIKU MBILI DIRISHA LA RUFAA

Dirisha la rufaa sasa kufungwa Ijumaa Novemba 12, 2021

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumatano Novemba 10, 2021) imetangaza kuongeza muda wa siku mbili zaidi hadi Novemba 12,2021 ili kuwawezesha wanafunzi wahitaji kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao.

Dirisha hili la rufaa linatoa nafasi kwa wanafunzi walioomba mkopo kwa mwaka 2021/2022 lakini hadi sasa hawajapangiwa mikopo au wamepangiwa viwango ambavyo wanahitaji kuongezewa, kuwasilisha maombi yao.

Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica Nyahende amesema uamuzi wa kuongeza muda umezingatia maoni ya wadau, wakiwemo wanafunzi, ambao walihitaji muda zaidi.

“Tulifungua dirisha siku ya Jumamosi (Novemba 6,2021) kufuatia maoni yaliyotolewa na wadau wetu tumeamua kuongeza muda wa siku mbili zaidi hadi Ijumaa, Novemba 12 mwaka huu ili kuendelea kutoa fursa kwa waombaji kuwasilisha rufaa zao” amesema Dkt. Nyahende.

Dkt. Nyahende amewataka waombaji mkopo kusoma maelekezo kwa umakini na kuyazingatia ikiwemo kuweka nyaraka zinazodhibitisha uhitaji wao ambazo awali hawakuziweka na kuongeza kuwa waombaji wote wanapaswa kutembelea akaunti zao walizotumia kuomba mikopo (SIPA) ili kupata taarifa za kina.

Serikali katika mwaka 2021/2022 imepanga kutoa mikopo kwa wanafunzi 160,000 ikiwemo wanafunzi 70,000 wa mwaka wa kwanza. Hadi sasa jumla ya wanafunzi 65,359 wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 169.3 bilioni.