Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


26
October 2021

15,261 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 37.9 BILIONI AWAMU YA TATU

Wanafunzi wapya waliopangiwa wafikia 60,356

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo (Jumanne, Oktoba 26, 2021) orodha ya Awamu ya Tatu yenye wanafunzi 15,261 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 37.9 bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaoanza wiki hii.

Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB Dkt. Veronica Nyahende amesema kuwa orodha hiyo iliyotolewa leo inafanya jumla ya wanafunzi wapya wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo kufikia 60,356 yenye thamani ya TZS 157.3 bilioni.

Dkt. Nyahende ameongeza kuwa HESLB tayari imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa awamu zote tatu katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) ili kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

Orodha ya Awamu ya Nne

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Nne, Dkt. Nyahende amesema itatolewa siku chache zijazo baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya tatu inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo kimoja. Tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutatoa orodha ya ya awamu ya nne siku chache zijazo,” amesema Dkt. Nyahende.

TZS 570 Bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2021/2022

Dkt. Nyahende amesema Serikali imetenga TZS 570 Bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka. 

Fedha zimeanza kutumwa vyuoni

Dkt. Nyahende amesema HESLB imeshapokea fedha na kukamilisha taratibu zote kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na fedha za awamu zote tatu zimeanza kutumwa vyuoni.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea fedha ili watimize ndoto zao,” amesema Dkt Nyahende.

Wito

HESLB inawasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Mwisho.

Imetolewa na:

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

DAR ES SALAAM

Jumanne, Oktoba 26, 2021