Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


2
August 2024

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU FURSA ZA 'SAMIA SCHOLARSHIPS'

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

TAARIFA KUHUSU FURSA ZA ‘SAMIA SCHOLARSHIPS’ KWA MWAKA WA MASOMO 2024/2025

1.0    UTANGULIZI

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatangaza programu ya Ufadhili iitwayo ‘SAMIA SCHOLARSHIPS’ kwa masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita wa mwaka 2024 ulioendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA na PMC). 

Ufadhili wa ‘SAMIA SCHOLARSHIPS’ utagharamia masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba kwa kuzingatia ‘Mwongozo’ unaotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambayo inasimamia utekelezaji wa skolashipu hizi. Mwongozo huo unapatikana katika www.heslb.go.tz

2.0    SIFA ZA KUPATA UFADHILI

Ufadhili huu utatolewa kwa wahitimu wa kidato cha sita wenye sifa zifuatazo:

i.       Awe Mtanzania;

ii.       Awe na ufaulu wa juu kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2024 iliyoendeshwa na NECTA katika tahasusi za sayansi zilizotajwa;

iii.       Awe amepata udahili katika Chuo cha Elimu ya Juu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali katika programu za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Tiba  ambazo zimetajwa katika kundi la kwanza (Cluster 1) katika Mwongozo wa utoaji mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2024/2025 unaopatikana kupitia www.heslb.go.tz

iv.       Awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa.

3.0    MAENEO YA UFADHILI

Ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya kugharamia maeneo yafuatayo:

a.       Ada ya Mafunzo;

b.       Posho ya chakula na malazi;

c.       Posho ya Vitabu na Viandikwa;

d.       Mahitaji Maalum ya Vitivo;

e.       Mafunzo kwa Vitendo;

f.        Utafiti;

g.       Vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu; na

h.        Bima ya Afya

4.0    MUDA WA UFADHILI

Wanafunzi watakaofadhiliwa, watagharimiwa kati ya miaka mitatu (03) hadi mitano (05) kulingana na programu husika walizodahiliwa.

5.0    UTARATIBU WA KUOMBA UFADHILI

‘Samia Scholarships’ yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao https://olas.heslb.go.tz ndani ya siku 23 kuanzia Agosti 08, 2024 hadi Agosti 31, 2024. Wanafunzi watakaoruhusiwa kuomba ni wale ambao orodha yao imetangazwa katika www.heslb.go.tz   

6.0    WAJIBU/MASHARTI YA UFADHILI

Mwanafunzi atakayepata ufadhili wa ‘SAMIA SCHOLARSHIPS’ atawajibika kuzingatia masharti yafuatayo:

a.       Anapaswa kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;

b.       Anapaswa kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya fedha atakazolipwa moja kwa moja;

c.       Mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;

d.       Mnufaika hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika;

e.       Ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwa HESLB kupitia kwa chuo chake alichodahiliwa na kujisajili;

f.       Iwapo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kitashuka chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo, ufadhili utasitishwa;

g.       Mnufaika anapaswa kujisajili katika Mfumo wa Usimamizi wa Wanafunzi (Students Management System) unaopatikana kupitia https://scholarships.moe.go.tz/

MUHIMU KUZINGATIA:

1.       Ufadhili huu ni wa asilimia mia moja ambao kikomo chake kitazingatia miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

2.       Orodha ya majina ya wanafunzi husika inapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mtendaji,

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

Ijumaa, Agosti 2, 2024

 

Taarifa hii inapatikana katika www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz