The United Republic of Tanzania
HIGHER EDUCATION STUDENTS' LOANS BOARD

KUFUNGWA KWA MAOMBI YA MIKOPO KWA MWAKA 2020/2021


Tunafahamisha wadau wote kuwa leo Alhamisi (Septemba 10, 2020) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa njia ya mtandao, litafungwa rasmi. Baada ya muda huo, usajili mpya kwa ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa.

Muda uliotolewa kuomba

Dirisha linafungwa baada ya kuwa wazi kwa siku 50, kuanzia Julai 21, mwaka huu na hadi saa 7:00 mchana wa leo (Alhamisi, Septemba 10, 2020) jumla ya maombi 92,947 yalikuwa yamesajiliwa na kupokelewa. Kati ya maombi hayo, maombi 7,500 yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.

 

Tunatoa wito kwa waombaji mikopo hawa 7,500 kukamilisha maombi hayo ifikapo Septemba 15, 2020 ili yaweze kujumuishwa kwenye tathmini na uchambuzi na hatimaye wale wenye sifa wapangiwe mikopo na kutimiza ndoto zao za kupata elimu ya juu.

Aidha, tunapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo kuwa baada ya kufungwa kwa dirisha leo, kazi inayoendelea ni uchambuzi na uhakiki wa maombi hayo na ifikapo Septemba 27, 2020, orodha ya waombaji wanaopaswa kurekebisha maombi yao itawekwa kwenye tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).

Mchango wa TPC na RITA

Kwa kuzingatia kuwa mchakato wa maombi ya mikopo unahusisha wadau mbalimbali, tumewasiliana na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kukubaliana kuwa wataendelea kupokea na kutuma HESLB maombi hata baada ya mfumo kufungwa.

Aidha, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wanakamilisha orodha ya vyeti vyote vya kuzaliwa na vifo vilivyohakikiwa ambayo itatumiwa na HESLB kufanya uchambuzi.

Bajeti ya fedha za mikopo kwa 2020/2021

Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga TZS 464 bilioni zitakazowanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000. Kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo. Mwaka 2019/2020 jumla ya TZS 450 bilioni zilitengwa na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119.

Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru,

Mkurugenzi Mtendaji,

Alhamisi, Septemba 10, 2020,

DAR ES SALAAM.