Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


16
October 2024

HESLB YAKUTANA NA MAAFISA MIKOPO VYUONI

Menejimenti ya HESLB leo Jumatano, Oktoba 16, 2024 imekuwa na kikao kazi na Maafisa wanaosimamia ofisi za mikopo ya wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya kati zaidi ya 150 kilichoanza jijini Arusha ili kujadili masuala yaliyojitokeza mwaka wa masomo 2023/2024 na kujiandaa kwa mwaka mpya wa masomo 2024/2025 ulioanza mwezi huu wa Oktoba, 2024.  

Kikao kazi hicho cha siku mbili kinachoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kimefunguliwa rasmi na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Charles Mkombachepa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda.

Awali, katika hotuba yake, Dkt. Mkombachepa amesifu jitihada za Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha inatoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wenye sifa ili waweze kufikia ndoto zao.

“Tuipongeze Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ili kuwasomesha vijana wa kitanzania … nimeambiwa mwaka huu kiasi cha TZS 787 bilioni kimetengwa kwa ajili ya kusomesha wanafunzi mwaka huu 2024/2025, kati yao zaidi ya 80,000 ni wa mwaka wa kwanza”.  

Licha ya kuzindua kikao kazi kati ya Menejimenti ya HESLB na Maafisa wanaosimamia ofisi za mikopo ya wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya kati, maafisa 25 wametunukiwa vyeti na ngao kwa kutambua utendaji wao uliojipambanua ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa za wanafunzi kwa wakati zikiwemo hati za malipo ya ada.

Wadau wengine wanaoshiriki katika kikao kazi hicho kitakachohitimishwa kesho Oktoba 17, 2024 ni pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Zanzibar (ZHESLB), viongozi wa Shirikisho la Wanafunzi TAHLISO na taasisi za fedha.

Menejimenti ya HESLB imekuwa ikifanya vikao kazi na maafisa wanaosimamia ofisi za mikopo vyuo tangu serikali ilipoanzisha ofisi hizo mwaka 2011 ili kila mara kuhakikisha wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu wanapata huduma stahiki.