Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


13
September 2024

HESLB na TRA kushirikiana utoaji na urejeshaji mikopo elimu ya juu

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Ijumaa Septemba 13, 2024) imebadilishana Hati za Ushirikiano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo utekelezaji wake unalenga kubadilishana taarifa ili kuboresha utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Hafla ya kubadilishana hati hizo imefanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na watendaji wakuu wa taasisi hizo mbili.

Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema lengo la ushirikiano na TRA ni kuboresha huduma za HESLB na kuwafikia wadau mbalimbali nchini nzima.

“Kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) tunaweza kutambua changamoto mbalimbali na hivyo sisi tukaboresha huduma zetu kwa mfano  kwenye Mikopo tunayoitoa, huduma tunazozitoa tunaweza tukaboresha kupitia mabadilishano ya Kanzidata kati ya taasisi hizi mbili”, amesema Dkt. Kiwia.

Aidha, Dkt. Kiwia ameongeza kuwa ushirikiano huo ni utekelezaji wa maagizo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka mifumo ya taasisi za serikali kusomana ifikapo Disemba mwaka huu.

‘“Jambo hili litaendana na agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo aliagiza taasisi za serikali mifumo yake yote isomane kabla ya Desemba mwaka 2024 na niseme kupitia vyombo vyenu vya habari kwamba  tutalikamilisha kikamilifu kabla ya kufika Desemba mwaka huu”,  amesema Dkt. Kiwia.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Yusuph Mwenda ameshukuru kwa taasisi yake kushirikishwa na kutoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kujitokeza na kuanza kurejesha ili kuwezesha kukopesha wanafunzi wengine wa kitanzania.

“Nawasihi wanufaika wa mikopo warejeshe sababu wao walipewa mikopo, kwakuwa kuna wengine walikopeshwa na wakarejesha’”, amesema Kamishna Mwenda.