Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumatano, Septemba 11, 2024) imebadilishana Hati za Makubaliano na taasisi tatu za kimkakati ambazo utekelezaji wake unalenga kubadilishana taarifa ili kuwasaka wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu.
Taasisi hizo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), CREDITINFO Tanzania Ltd ambayo ni taasisi ya uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo katika taasisi za fedha.
Hafla ya kubadilishana hati hizo imefanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na watendaji wakuu wa taasisi hizo.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema lengo la ushirikiano na taasisi hizo ni kuongeza kasi ya kuwasaka wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu hususan waliopo katika sekta binafsi na isiyo rasmi kwa kutumia kanzidata na mifumo ya TEHAMA iliyounganishwa.
“Katika kazi yetu ya kukusanya fedha za mikopo, tunawahitaji wadau hawa … hivyo tunaomba mtufikishie ujumbe kwa wateja wetu kuwa sasa tunakwenda kufanya kazi na wadau watatu, na wengine tutawatangazia siku chache zijazo … tunalenga kuwafikia wadaiwa wote kwa kutumia mifumo,” amesema Dkt. Kiwia.
Wakizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Deusdedit Buberwa wameahidi kutekeleza wajibu wao katika makubaliano hayo na kufafanua kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha taasisi za Serikali zinaunganisha mifumo yao ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CREDITINFO, Edwin Urasa ameshukuru kwa taasisi yake kushirikishwa na kutoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kujitokeza na kuanza kurejesha ili kujijengea uaminifu wa kukopesheka na taasisi za fedha.
“Hili ni jambo jema kama mteja ni mlipaji mzuri, lakini kama si mlipaji mzuri ni vema ukaanza kulipa madeni yako ukiwemo mkopo wa elimu ya juu kwa sababu sisi tuna taarifa za wakopaji kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo HESLB … na tunafanya kazi kwa kuzingatia sheria,” amesema Urasa.
HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na hadi sasa jumla ya watanzania 754,000 wamekopeshwa TZS 7.2 trilioni. Kati ya fedha hizo zilizotolewa, TZS 2.1 trilioni zimeiva na zilizokusanywa ni TZS 1.5 trilioni sawa na asilimia 71.