Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


5
June 2023

HESLB YAWAPA ZAWADI WAAJIRI BORA SEKTA BINAFSI DAR

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) leo (Jumatatu, Juni 5, 2023) imewatambua na kuwapa tuzo maalum waajiri 10 kutoka mkoa wa Dar es salaam kutokana na kuwasilisha kwa wakati makato ya wafanyakazi wao waliokopeshwa mikopo ya elimu ya juu.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi ngao, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, amesema waajiri hao wamekuwa mfano kwani wamekuwa wakikata kwa wakati fedha za wafanyakazi wao kiasi cha asilimia 15 ya mshahara na kuwasilisha HESLB kupitia Mfumo wa Ki-elektroniki wa Malipo ya Serikali (GePG).

“Tunathamini sana ushirikiano tunaopata kutoka kwa waajiri na ndiyo sababu tumeamua kuwatambua waajiri hawa kutoka sekta binafsi ili kuwahamasisha waajiri wengine ambao utekelezaji wao wa masharti ya Sheria ya HESLB hauridhishi kama inavyotarajiwa,” amesema Badru katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kuongeza:

“Kwa mkoa wa Dar es salaam pekee, kati ya Julai 2022 hadi Mei 2023 tumekusanya TZS 17 bilioni kutoka sekta binafsi ambayo ni sawa na asilimia 22.3 ya jumla ya TZS 76 bilioni tunazokusanya kwa mwaka kutoka sekta binafsi nchini kote … hivyo tumekutana kuwashukuru kwa kutuunga mkono,” amesema Badru na kufafanua kuwa wataendelea kuwatambua waajiri katika mikoa mingine.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa HESLB Kanda ya Dar es salaam Anna Sabuni amewataja waajiri hao bora zaidi kwa mkoa wa Dar es salaam ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); Benki ya Diamond Trust; Kampuni ya Coca Cola Kwanza; na Shule za Feza.

Waajiri wengine ni Kampuni ya Bia Serengeti; Kampuni ya SICPA Tanzania; Taasisi ya Kifedha ya Brac Ltd; Taasisi ya Afya Ifakara (IHI); Kampuni ya Simu ya Viettel (Halotel) Tanzania; na Shirika la GIZ.

“Ofisi yetu ya Kanda ya Dar es salaam ilianzishwa mwezi Novemba 2021 na hadi Juni 2022, tuliweza kukusanya TZS 12 bilioni kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi na tumeona tunaweza kukusanya zaidi tukiendeleza ushirikiano,” amesema Anna Sabuni.

Akizungumza katika hafla hiyo wa niaba ya waajiri, Mkurugenzi Mktendaji wa Taasisi ya Afya ya Ifakara Dkt. Honorati Masanja aimeshukuru HESLB kwa kuandaa hafla hiyo na kushauri HESLB kuandaa mikakati ya kuwafikia waajiri wasiotii masharti ya sheria ili kuwaelimisha.

“Sisi tuilioalikwa tunatii na kutekeleza masharti ya sheria ya HESLB … sasa ni vema utaratibu kama huu ukafanywa kwa waajiri wasiotimiza masharti ili wabadilike baada ya kuelimishwa,” amesema Dkt. Masanja.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwaka 2005 ikiwa na majukumu kadhaa, lakini makuu mawili – kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa kitanzania waliopata nafasi za kujiunga na taasisi za elimu ya juu; na kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.