Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


17
March 2023

Dkt. Rwezimula: Tafakuri Ugharimiaji Elimu ya Juu ni Muhimu

Serikali inaendelea kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa sasa wa ugharimiaji wa elimu ya juu ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kuhimili ongezeko la wanafunzi wa elimu ya juu watakaotokana na sera ya elimu ya msingi na sekondari bila ada.

Akiongea katika ufunguzi wa Kongamano la Tafakuri ya Ugharimiaji wa Elimu ya Juu jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Jasson Rwezimula amesema tafakuri kuhusu mfumo wa sasa wa ugharimiaji ni muhimu kwa kuwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu wanaongezeka kila mwaka.

“Nimatumaini yangu kuwa majadiliano na tafakuri kutoka katika mkutano huu yatatoa mchango muhimu katika safari yetu ya kubadilisha mpango wa ufadhili wa elimu ya juu,” amesema Dkt. Rwezimula katika kongamano hilo lililoandaliwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kufanyika Alhamisi, Machi 16, 2023 katika Hoteli ya Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.

Kongamano hilo limeshirikisha wadau wa elimu ya juu, zikiwemo taasisi za elimu ya juu, wanafunzi, sekta binafsi, taasisi za fedha na waajiri ambao walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu maboresho ya ugharamiaji wa elimu ya juu nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB Prof. Hamisi Dihenga amesema katika miaka 18 ya kuwepo kwa HESLB kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu huku serikali ikiwa ni mfadhili mkuu.

“Tumeona tuje na mjadala wa kuangalia namna ya ufadhili kuwa endelevu na kuibua vyanzo vingine, hii ni kujiandaa katika kupokea idadi kubwa ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo kutokana na sera ya elimu ya ada bila malipo,’’ alieleza Prof. Dihenga.

Katika kongamano hilo, mada kuu tatu ziliwasilishwa na kujadiliwa ambazo ni Ukusanyaji wa Rasilimali kwa Ugharamiaji wa elimu ya juu, Athari za Kijamii na Kiuchumi Zinazotakana na Ugharimiaji wa Elimu ya Juu na Usimamizi na Vipaumbele katika Ugharimiaji wa Elimu ya Juu.

Tangu kuanza kutolewa kwa mikopo mwaka 1994/1995, Serikali imetoa mikopo ya elimu ya juu yenye jumla ya thamani ya TZS 5.37 trilioni kwa wanufaika 654,919.